Masai Wa Kigoma Afunguka Uhusiano Wake Na Wema Sepetu



Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nyembo Ayoub ‘ Masai wa Kigoma’

Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nyembo Ayoub ‘Masai wa Kigoma’ amefunguka uhusiano wake na mwanadada Wema Sepetu, baada ya kupeleka posa na kushindwa kumuoa mwanadada huyo.

Akizungumza na Hivisasa blog, amesema kuwa alikuwa na mapenzi ya kweli kwa mrembo Wema, alihisi ni mwanamke ambaye anahitaji mume baada ya kutendwa na wanaume kadhaa.

“Wema ni mwanamke ambaye nilimpenda na nilimuonea huruma sana kwa mrembo kama yule kuteseka na mapenzi, nikaona ni bora nimpose na kumuoa kusudi apate kuonja mapenzi yasiyo ya udanganyifu,” alisema Masai

Amesema kuwa ingawa hakuwahi kumfahamu kiundani alichukua nafasi hiyo kama ilivyo kuwa mila na desturi za kiafrika kuwa ukimpenda mtu unatuma mshenga na wazazi wakikubali unaoa.

Amesema lakini mambo yalikuwa tofauti kwa mwanadada huyo kumbe alikuwa hajamaliza ujana wake na hivyo kuendelea kupapatika na watu wenye fedha zao ambao walikuwa hawampi mapenzi ya kweli na hivyo kumkosa.

Amesema kuwa kwa kuwa hakumpa nafasi ya kuwa mpenzi wake sasa amepata mwanamke ambaye ameshamtolea posa bado tu kukamilisha mahari na kufunga ndoa.

Aidha, amewataka wanawake kuwa na misimamo na kujiheshimu kwa kuwa na watu wenye msaada na sio kuwa na wapenzi kwa ajili ya fedha zao na kujikuta wakilia kila siku.