INAKUHUSU: WANAWAKE WENGI WAKIVIKOSA HIVI LAZIMA WASEPE



Kama mwanaume lazima upate wakati

wa kujua unatakiwa kufanya nini kwa
ajili ya kulifanya penzi lako lizidi
kuchanua.
USAFI BINAFSI
Asilimia kubwa ya wanawake
wanapenda sana usafi. Ni aghalabu sana
kukutana na mwanamke asiyejipenda.
Ndiyo maana wanaitwa mapambo ya
nyumba au la nyumba! Ni kwa sababu
ya hulka yao ya kupenda sana usafi.
Mwanamke anavutiwa sana na
mwanaume mtanashati. Usafi wako
unamfanya ajiamini kuwa na wewe.
Hata nyumbani kwako, lazima uishi
katika nyumba safi. Hata anapokuja
kukutembelea, anakuta mazingira
masafi kuanzia sebuleni hadi chumbani.
Anapokukuta katika hali ya usafi,
inakuwa rahisi zaidi yeye kuanzia hapo
alipokukuta na kuendelea mbele.
KUJIAMINI
Mwnamke anajisikia salama zaidi akiwa
na mwanaume ambaye anajiamini –
mwenye uwezo wa kutetea hoja zake na
kujieleza sawia. Siyo anayebabaika. Suala
la msimamo binafsi, kwa mwanamke ni
kubwa kuliko hata kumnunulia
manukato mapya!
Mathalani unakuwa naye katika mtoko,
angependa kukuona ukiwa katika hali
halisi ya maisha yako, usiyeyumbishwa
na mwenye kutoa maamuzi
yasiyoyumba.
Wakati mwingine, mwanamke anaweza
kukupima hata katika jambo ambalo
amekosea yeye, ataangalia unavyotoa
maamuzi yako, lakini pia atafuatilia
kuona kama utakuwa mwepesi wa
kuyabadilisha.
Anataka kuona msimamo wako muda
wote. Mwenye kujiamini na mawazo
yasiyo na matege wala makengeza!
KUJITETEA
Kipengele hiki hakina tofauti kubwa
sana na kilichopita, lakini hapa ni
kwenye upande wa kujitetea zaidi.
Wakati unapodai haki yako mbele ya
mwanamke wako, suala la kujitetea
linapewa nafasi kubwa sana.
Wanawake hawapendi kuwa na
wanaume ambao wapo tayari kuonewa.
Wanataka wenye uwezo wa kusimama
kidete kuona haki zao hazichukuliwi
kirahisi.
Hili si suala la kutetea tu haki yako pekee
kama mwanaume, bali inapobidi
kusimamia haki ya mwanamke wako.
Nisieleweke vibaya katika hili, lakini
mwanaume imara ni yule ambaye ana
nguvu – anafanya mazoezi na ambaye
yupo tayari kwa lolote!
Inapowezekana, uwe na uwezo wa
'kuzichapa' ikiwa mtakutana na vibaka
au watu wabaya wenye lengo wa
kukudhuru/kuwadhuru au kumdhuru
mpenzi wako.
Mwanaume aliye 'fiti' ni chaguo la
wanawake wengi. Si mnyonge. Mpole
kupitiliza na aliye tayari kuonewa! Huyu
hana nafasi.
KUJALI
Wanawake wanapenda sana wanaume
wanaojali. Wanawaona wao ni kila kitu
na wanaotoa kipaumbele kwao. Kama
huna tabia hiyo, ujue upo katika nafasi
kubwa ya kumkwaza mpenzi wako. Mjali
mpenzi wako kwa kila hali.
Kumjulia hali kila wakati na kutaka kujua
maendeleo yake, kutakupa nafasi kubwa
sana ya kuendelea kudumu katika
uhusiano hai.
UKARIBU
Kati ya vitu vinavyowapa mshawasha
mkubwa wanawake ni pamoja na
kusogezwa karibu. Hapa ni kuwa naye
katika mambo mengi unayoyafanya kila
siku.
Ni vizuri kuwasiliana naye mchana,
ukitaka kujua aina ya chakula alichokula
siku hiyo au ikiwezekana mchagulie. Ni
mambo madogo sana lakini
yanayoongeza nakshi katika mapenzi.
Yapo mengi sana ambayo kwa
kuyafanya utakuwa umemsogeza
mpenzi wako karibu yako. Hebu tumia
ubunifu wako ili uweze kuteka hisia za
mwenzi wako kisawasawa!
KUMSIFIA
Wanaume wengi hupuuzia hili, huona
kama ni jambo lisilo na maana sana
kwao na wenzi wao. Hali ni tofauti sana
kwa wanawake ambao hupenda
kuwasifia wanaume zao. Nitakupa
mifano miwili ya namna wanandoa wa
jinsia mbili tofauti
wanavyotambulishana kwa jamaa zao.
MWANAUME: "Peter kutana na mke
wangu, anaitwa mama Diana. Nipo naye
mwaka wa tatu sasa, tuna watoto
wawili, huyo Diana na mwingine
anaitwa Cris. Mama Diana, huyu ni Peter
nilisoma naye A – Level, Tosamaganga
Sekondari."
MWANAMKE: "Suzan, huyu ndiye mume
wangu mpenzi...anaitwa Elifaraja lakini
mimi napenda zaidi kumuita Elly.
Kiukweli nampenda sana mume wangu
jamani, tuna mtoto wetu mmoja,
anaitwa Agness. (Akimgeukia mumewe)
Baby, huyu hapa ni rafiki yangu Suzan.
Yaani tumekua naye mtaa mmoja huko
Arusha."
ANGALIA TOFAUTI
Bila shaka kwa namna wawili hao
walivyotambulishana unaweza kuona
tofauti kubwa. Mwanaume
amemtambulisha mkewe kawaida
kabisa, hajaonesha manjonjo au namna
anavyompenda na kumthamini
mwenzake, lakini mwanamke amefanya
hivyo.
Sikia nikuambie, KUMSIFIA mwanamke,
kuna nafasi kubwa sana kwake.
Chunguza kwa makini, hata
kunapokuwa na mgongano katika
familia, halafu wakatokea wageni, baada
ya utambulisho na mazungumzo ya
hapa na pale, wageni wakiondoka
kunakuwa na uwezekano mkubwa zaidi
wa kumaliza mpasuko katika familia.
Jenga utamaduni wa kumsifia mpenzi
wako, unamuweka katika kilele cha
upendo. Anajiona kamili, peke yake na
mwenye nguvu kwako. Anajiamini na
unamfanya azidi kukupenda kwa kuwa
anaamini yupo na mwanaume ambaye
anajivunia kuwa naye.
MALENGO
Wanaume wengi wana ulemavu mmoja;
hawapendi kuwashirikisha wanawake
katika mambo yao. Wanapenda kufanya
mambo yao kwa siri na wakati
mwingine ikilazimika kumwambia
mkewe basi kwa mshtukizo baada ya
kukamilisha jambo husika.
Hii si sahihi. Dunia ya leo imebadilika
rafiki zangu. Inawezekana wazee wa
zamani walikuwa sahihi, maana ilikuwa
ni suala la kununua ng'ombe na
kuwaweka katika zizi kwenye kijiji cha
jirani, halafu wanapewa malisho mazuri,
baada ya miaka miwili wanazaliana,
hapo ndipo anamweleza mkewe.
Siku hizi dunia imebadilika, kuna mambo
mengi. Kuna suala la hasara katika
biashara, utapeli n.k. Mkeo ndiye rafiki
yako mkubwa kuliko wote, ndiye ndugu
yako wa karibu zaidi kuliko yeyote. Yes!
Mkeo ndiye ndugu yako maana
umetengeneza naye familia.
Mmeshirikiana kuzaa watoto na kujenga
maisha pamoja.
Yeye anapaswa kujua mambo yako,
ndiye mtetezi wako nambari wani.
Mweleze juu ya malengo yako, wakati
mwingine anaweza kukusaidia sehemu
ambayo hukutarajia.
Hata hivyo, kumshirikisha katika
malengo yako, kunampa nguvu na
nafasi ya kujiona mama katika familia
yenu. Msaidizi kamili wa nyumba yenu.
KIPAUMBELE
Kuna wakati wanawake huwa na
mambo yao binafsi. Kazini au kifamilia.
Inawezekana akatatizika katika eneo
fulani ambalo kwa namna moja ama
nyingine atahitaji usaidizi wako. Ikitokea
mkeo akawa katika hali hiyo, msikilize.
Mathalani ana tatizo la kifamilia,
amekuambia mmoja wa wazazi wake
anaumwa, msaidie. Si lazima kifedha,
lakini kuonesha kujali kwako tu,
kutampa matumani kwamba anaishi na
mtu sahihi. Acha kupuuza mambo yake;
hata yale madogo, kama ya 'mtoto wa
dada amerudishwa ada shuleni'.
Msikilize, mshauri panapofaa kufanya
hivyo na ukiweza msaidie hata kifedha.
Katika upande wa pili ni hivyo hivyo.
Labda una tatizo binafsi, kazini kwako
au kifamilia, mshirikishe.
Unaweza kushangaa jambo ambalo
uliamini unaweza kulimaliza peke yako,
kwa kumshirikisha likawa jepesi zaidi na
mambo yakaendelea vyema. Kipaumbele
kwa namna yoyote ile, kunaongeza
mapenzi zaidi kwa mwanamke.
TENDO LA NDOA
Hiki ni kipengele nyeti, kinachohitaji
lugha nzuri ya kirafiki kukifafanua.
Hakuna siri, tendo la ndoa ni moja ya
kiwakilishi cha ndoa. Maana hata
maandiko yanasema: "Mwanamke
ataacha wazazi wake na kwenda kwa
mumewe, nao watakuwa mwili mmoja."
Kimsingi tendo la ndoa lina nafasi yake.
Ni muhimu likaheshimiwa na
kutengewa muda maalum wa kufurahia.
Si papara. Kwa bahati mbaya wanaume
huwa si wafuatiliaji sana wa kujua
namna ya kuwafurahisha zaidi wenzao.
Wenyewe wanajiwazia wenyewe.
Wanafikiria namna ya kuwakomoa
wenzao.
Si sahihi.
Tendo la ndoa halina maana ya
kukomoana. Jenga mazoea ya kufanya
maandalizi kamili kabla ya tendo. Sikiliza
hisia za mwenzako. Ukiweza kumjulia
mke wako katika eneo hili, ni wazi
kwamba utazidisha upendo wake
kwako, lakini pia atakuwa katika kuta za
uaminifu. Akatafute nini nje wakati
wewe ndiye mganga wake unayeweza
kumtibu barabara?
Kuna kitu nimesahau kweli? Kama kipo
nitafute pembeni, kwa hapa haya
yatoshe kukufanya uelewe nilichotaka
kukuelekeza. Nikuache na neno moja;
uamuzi wa kuijenga ndoa yako upo
mikononi mwako. Ukitaka iwe
shaghalabaghala, pia ni wewe tu!