AKUTANA NA WEMA SEPETU KWENYE DUKA LA SAMAKI



WIKI iliyopita tuliishia pale ambapo mrembo wa kijijini kwa kina marehemu Kanumba alivyopagawa baada ya kumuona mwigizaji huyo katika runinga akiigiza michezo mbalimbali na kuonesha nia ya kukubali ombi la Kanumba.
Kanumba naye alimkataa kwani alijua amejirahisisha kwa sababu ya umaarufu na si penzi la dhati, akamchomolea.SASA ENDELEA...

Mwaka 2006 alijiunga katika Kampuni ya Mtitu Game First Quality ambapo aliweza kucheza sinema kama She is Johari, My Sister, Dar To Lagos, Cros My Sin, The Director na Hero of The Church.
Kupitia sinema mbalimbali alizocheza nje na wasanii wa nje ya nchi, Kanumba aliweza kuigiza pamoja na vigogo wa sinema kama Mercy Johnson, Nkiru Silvanus, Femi Ogedegbe na Ramsey Nuoah.

AKUTANA NA WEMA SEPETU
Mara baada ya kufanya kazi mbalimbali na Kampuni ya Mtitu, Kanumba alikutana na Wema Sepetu (wakati huo alikuwa mshindi wa Miss Tanzania 2006).Wema baada ya kushinda Taji la Miss Tanzania, alipata pia fursa ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya dunia nchini Poland. Aliporejea tu nchini, alikutana na Kanumba ambaye walianzisha urafiki.

ILIKUWAJE?
Wema na Kanumba walikutana kwa bahati mbaya tu. Wema alikuwa na dada yake katika duka moja la samaki lililopo jijini Dar. Walipofika katika duka hilo, walikuta kuna purukushani za wasanii walikuwa wakirekodi sinema ya Kanumba iitwayo Lost Twins.

Kila mtu kwenye duka hilo alikuwa makini kushangaa kile kilichokuwa kinaendelea ambapo Kanumba na waigizaji wenzake walikuwa bize na kazi yao hali ambayo ilimfanya Wema na dada yake pia kutazama shughuli hiyo badala ya kununua samaki.

Wakati zoezi la kurekodi likiendelea, Wema alikuwa akimtambua vyema Kanumba kutokana na umaarufu wake lakini pia Kanumba aliweza kumtambua Wema kwani naye pia alikuwa maarufu tayari kupitia shindano la urembo la Miss Tanzania.

Kuna wakati walikodoleana macho kwa muda, wote wakashusha tabasamu la kuonesha wanafahamiana.
Baada ya muda fulani, Kanumba alijikuta amelazimika kuacha zoezi la kurekodi na kwenda katika eneo ambalo Wema alikuwa amesimama. Walisalimiana na kuahidiana kukutana baada ya kumaliza shughuli hiyo.Baadaye wawili hao walikutana kama marafiki wapya. Kanumba tayari alikuwa ameshampenda Wema, akaanza kummwagia sifa mrembo huyo aliyekuwa akionekana na sura ya upole.

Wakati huo Wema hakuwa na haraka ya kuzungumza lolote na Kanumba kwa kuwa alikuwa na hofu ya kufuatwa na kamera za vyombo vya habari.Bila kupoteza muda, Kanumba alianza na gia ya kumshawishi Wema ajiunge na uigizaji. Wema hakukubali ila alimweleza alihitaji kuwaomba ruhusa wazee wake.

Kitendo tu cha Wema kukubali kwenda kuomba ruhusa kwa wazazi, kilimfurahisha sana Kanumba.
Walibadilishana namba za simu, wakaahidiana kutafutana wakati wowote. Wema naye pia alifurahia sana kukutana na Kanumba kwani alikuwa amezoea kumuona kwenye runinga tu.Kanumba akilini mwake tayari alikuwa na wazo la kufanya sinema ya pamoja na mrembo huyo.Wakapigiana simu siku nyingine na kupanga mkutano mwingine baina yao.