Dalili za mwanamke anayetoka nje ya ndoa



Wataalamu wa maswala ya mahusiano wanaamini kwamba, mwanamke anapotoka nje ya ndoa yake, inakuwa rahisi sana kubainika au kufumaniwa kuliko ilivyo kwa mwanaume.

Hii inatokana na ukweli kwamba, hisia zinakuwa na nafasi kubwa sana kwa mwanamke, kwani mwanamke huishi kwa hisia zaidi kuliko mwanaume. Bado nasisitiza kwamba, haipaswi na siyo sahihi mtu kuchukulia dalili hizi kama ushahidi wa mpenzi wake kutoka nje ya ndoa. Uchunguzi wa kina kufuatia dalili hizi ni muhimu sana.

Zifuatazo hapa chini ni baadhi ya dalili zinazoweza kuonyeshwa na mwanamke ambaye anatoka au yupo kwenye harakati za kutoka nje ya ndoa yake:

1.KUCHELEWA: Kuna wakati mwanamke anaweza kuaga kwamba anakwenda saluni au kusuka, badala ya kurejea kwa muda ambao umezoeleka, anachukua muda mrefu hata mara tatu zaidi. kuna wakati kwenda sokoni huchukua saa kadhaa bila kujali soko liko umbali gani. Kama ni mara moja sawa, lakini ikishakuwa zaidi ya mara moja huenda kuna tatizo la kukosa uaminifu.

2.KUBADILI MAENEO: Hebu chukulia kwamba, mwanamke amezoea kwenda soko fulani la karibu, hospitali fulani ya karibu, saluni fulani ya karibu na hata nyumba fulani ya ibada ya karibu. Unapoona anahama maeneo ya karibu ya huduma na kwenda ya mbali, bila sababu ya msingi, huna budi kuanza kutuhumu mwenendo mbaya.

Siyo lazima kuhama kokote kuwe na mwenendo mbaya, lakini kama kuhama kwenyewe kunatia shaka kwa sababu maelezo ya kuhama huko hayana msingi, mwanaume ana kila sababu ya kuchunguza kama hakuna usaliti unao anywa.

3.UNUNUZI USIO WA KAWAIDA: Kama mwanamke anatoka nje ya ndoa yake kwa ajili ya kupata fedha, basi atakuwa na mabadiliko makubwa katika mtindo wake wa manunuzi.
Atakuwa ananunua vitu vya thamani kubwa kuliko uwezo wake, atakuwa na fedha nyingi tofauti na ambazo angekuwa nazo na pengine kumiliki mali kama nyumba kwa siri.

4.KUANZISHA VURUGU: Kuna wakati mwanamke anayetoka nje ya ndoa huanzisha vurugu za makusudi na mumewe. Lengo la kuanzisha vurugu hizo ni ili apate nafasi ya kujifanya amezira na kuondoka nyumbani kwa muda.

Huo muda anapoondoka nyumbani kujifanya kakerwa na vurugu hizo ndiyo muda ambao anautumia kwenda kwa hawara yake.

5.KUSITISHA UAMINIFU: Mwanamke anayetoka nje ya ndoa, mara nyingi husimamisha kumwamini mumewe, yaani hayuko tayari kushiriki masuala ya siri, ambayo wanandoa huwa wanashiriki.

Husita kumshirikisha mumewe kwenye mambo yake mengi. Lakini pia husita kumuomba mumewe ushauri, kama alivyokuwa akifanya siku za nyuma.

6.KUACHA KUVAA PETE: Kuna sababu nyingi ni kwa nini mwanamke anaweza kuacha kuvaa pete yake ya ndoa. Moja ya sababu hizo ni kusalitiwa na mumewe au ndoa yake kuwa kwenye misukosuko mikubwa sana.
Lakini nje ya misukosuko mikubwa ya ndoa, sababu nyingine inayoweza kumpelekea mwanamke kuvua mara kwa mara au moja kwa moja pete yake ya ndoa, ni kuwa na uhusiano nje ya ndoa yake.

7.KUONESHA WASIWASI: Kama mwanamke anatoka nje ya ndoa yake , ni lazima atakuwa na wasiwasi na mashaka yasiyo na sababu mbele ya mume wake.

Anaweza kuonesha kutotulia kwa aina fulani kana kwamba, anahofia kuna siri itatoka au kuna kitu ambacho tayari mume wake anakijua dhidi yake. Mara nyingi wasiwasi na mashaka humtawala sana mwanamke anayetoka nje , hasa katika hatua zake za awali za kutoka nje.

8.KUZUNGUMZIA KUACHWA: Kuna wakati mwanamke anaweza kuwa anatoa kauli za kuonesha kwamba, kama mwanaume anaona vipi , wanaweza kuachana.

Kama kila penye ugomvi kidogo tu mwanamke anakimbilia kusema, “kama ni kuachana, tuachane tu” hiyo inaweza kuwa ni dalili mbaya kwa mwanamke anayetoka nje ya ndoa kwa sababu hana tena upendo na mumewe.