MZIMU WA KANUMBA WADAIWA KUUWA WAWILI ENDELEA KUSOMA ZAIDI

HII ni habari ya kutisha! Takriban miaka mitatu imekatika tangu kifo cha aliyekuwa staa wa Bongo Movies, Steven Kanumba huku watu wawili wakifariki dunia kwa nyakati tofauti lakini nyuma ya pazia ya vifo vyao, mzimu wa Kanumba unatajwa kuhusika kutokana na watu hao kutaka kuishi mahali pa marehemu huyo

Aliyekuwa staa wa Bongo Movies, marehemu Steven Kanumba.
SOMA TUKIO HILI LA KUSHANGAZA
Itakumbukwa kwamba, baada ya kifo cha Kanumba, mama yake mzazi, Flora Mtegoa ndiye aliyeshika jukumu la kusimamia mali za marehemu mtoto wake (alikuwa na haki).
Miongoni mwa mali hizo ukiachilia mbali, magari, vifaa vya kurekodia filamu, viwanja na filamu zilizokuwa hazijalipwa, mama Kanumba aliimiliki ofisi ya Kanumba iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Kanumba The Great Film iliyokuwa Sinza.Hata hivyo, hivi mapema Februari, mwaka huu, mama Kanumba alitoa vitu kwenye ofisi hiyo kwa madai ya kushindwa kulipa pango, hivyo ofisi ikawa wazi.
KILICHOTOKEA SASA
Habari ambazo gazeti hili ilizipata zilidai kwamba, mpangaji mwingine aliikodisha ofisi hiyo kwa mkataba wa mwaka mmoja lakini hivi karibuni mtu huyo amefariki dunia.Msikilize shuhuda: “Kuna jamaa alipanga kwenye ofisi iliyokuwa ya Kanumba mara tu baada ya mama Kanumba kuondoka vitu kwa kushindwa kulipia mkataba mpya.
“Huyo jamaa alikuwa anahusika na masuala ya ujenzi. Jamaa alilipia kodi ya mwaka mmoja, akawalipa watu wamfanyie usafi yeye akaenda ‘saiti’ kwenye mambo yake ya ujenzi. Inadaiwa akiwa kule, kuna ‘kijiko’  kilichokuwa kinachimba kiwanja, bahati mbaya kikarudi nyuma na kumgonga, akaanguka na kufariki dunia.”
JE, NI MZIMU WA KANUMBA?
Kifo cha mtu huyo ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, kinaunganishwa na tukio lilitokea mwaka juzi baada ya kifo cha Kanumba kilichotokea  Aprili 7, mwaka 2012.Mara baada ya Kanumba kufariki dunia ghafla, mwanamke mmoja alikwenda kupanga nyumba ile aliyokuwa akiishi marehemu iliyopo Sinza, Dar, naye alifariki dunia ghafla.
MAJIRANI WALIZUNGUMZA
Wakati wa tukio hilo, wanahabari wetu walifika nyumbani kwa mwigizaji huyo ambapo walizungumza na majirani wakaelezea juu ya uwepo wa tukio hilo.Walisema japo hawaamini juu ya imani za masuala ya mzimu wa marehemu lakini kitendo cha mwanamke huyo kufariki dunia muda mfupi baada ya Kanumba kufa kiliwafanya washtuke na kuamini kwamba huenda ni mzimu wa Kanumba ndiyo ulichukua roho ya mpangaji huyo.
Mama Kanumba, Flora Mtegoa.
WENGINE WALIAMINI HIVI
Hata hivyo, baadhi ya watu wengine pia walisema yao wakidai kwamba, wanaamini kifo cha mwanamke huyo ni cha kawaida kama ilivyo kwa vifo vingine.“Kama siku za Kanumba zilivyokuwa zimewadia na huyo mpangaji pia siku zake zilikuwa zimefika ndiyo maana amefariki dunia,” alisema mmoja wa majirani.
ALIVYOSEMA MZEE ALIYEKULA CHUMVI NYINGI
Mzee mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mohamed Sumali (76), mkazi wa Mabibo-Relini, Dar akizungumza na gazeti hili kuhusu mazingira ya vifo hivyo, alisema:“Ipo mizimu ya hivyo. Mtu akifa, wa kwanza kuhamia kwenye nyumba aliyokuwa akiishi marehemu naye anakufa. Lakini si kwamba nyumba ndiyo ina mizimu. Kama hivyo vifo vimetokea kweli basi na mzimu wa Kanumba umeshaondoka.”
MAMA KANUMBA AZUNGUMZA
Baada ya kuzipata habari hizo, mwanahabari wetu alimvutia waya mama Kanumba kutaka kujua kama anajua lolote juu ya marehemu mtoto wake kuacha mzimu ambao unahusishwa na vifo hivyo ambapo alikiri kusikia taarifa za kifo cha jamaa aliyepanga kwenye ofisi za Kanumba lakini akasema hata yeye hajui sababu za kifo chake.
“Hata mimi nimesikia,  lakini sielewi chochote kuhusiana na mtu huyo kufariki dunia. Imenishtua kwa kweli maana si unakumbuka hata kule alikopanga (Kanumba) mwanzoni nako aliyepanga ile nyumba naye alifariki? Sijui hata ni kwa nini?” alihoji mama Kanumba kwa sauti iliyoashiria kushangaa sana.